Thursday, 22 March 2018

Hivi Ndio Viwango Vya Makato ya Kodi ya Mishahara ya Waajiriwa


MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) imefafanua kuhusu viwango vya kodi, anavyopaswa kukatwa mtu binafsi aliyeajiriwa.
Tokeo la picha la tra

Kiwango cha kodi, ambacho mtu anatakiwa kukatwa kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato, vinatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kulingana na kiwango cha kipato anachopata mtu kwa mwezi.

Ufafanuzi kuhusu kodi ya ajira, ambayo mwajiriwa anakatwa kwenye mapato au mafao yake, kiwango cha mshahara au kipato au ujira, kinachotakiwa kukatwa kodi ni kile kinachozidi  Tshs 170,000 kwa mwezi.

Kwa kuwa kwenye ajira kuna vyanzo tofauti tofauti vya mapato kwa mwajiriwa, kama vile motisha (bonus), kamisheni, ujira, mshahara, malipo ya likizo, posho na mengineyo, ambayo yote yakijumlishwa yanatengeneza kipato cha mwezi, hivyo kipato hicho kama hakizidi Tshs  170,000 hakikatwi kodi.

Kipato cha Shilingi Tshs 170,000 kushuka chini hakina kodi, kimesamehewa kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato Kifungu namba 10 ukisoma pamoja na jedwali la pili la kodi ya mapato ambalo linaonesha viwango vilivyosamehewa kodi kuwa ni pamoja na hiki cha Tshs  170,000 kushuka chini.

Kiwango kinachozidi Tshs  170,000 lakini hakizidi Tshs  360,000 kwa mwezi, kodi yake ni asilimia 9%. Kwa mfano mtu analipwa Tshs 240,000/=, kinachofanyika ni kwamba inatolewa Tshs 170,000 kwenye kipato hicho na kiasi kinachobaki ndiyo kinakatwa kodi ya asilimia 9%.

TRA inasema kuwa kwa mwajiriwa anayepata kipato kinachozidi Tshs  360,000 lakini hakizidi Tshs  540,000 kwa mwezi, kodi yake ni Tshs  17,100/=, lakini inajumlishwa na asilimia 20% ya kodi kwa kipato kinachozidi Tshs  360,000.

Vivyo hivyo kwa kipato kinachozidi Tshs 540,000 lakini hakizidi Tshs 720,000 kwa mwezi, kodi yake ni Tshs  53,100, lakini itaongezwa na asilimia 25% ya kiwango kinachozidi Tshs  540,000.

Kiwango chochote cha kipato cha kuanzia Tshs 720,000 kwenda juu kwa mwezi, kodi yake ni Tshs  98,100, lakini inajumlishwa na asilimia 30% ya kiwango kinachozidi Tshs  720,000, hivyo kodi kwa mtu binafsi hata kama analipwa Tshs  milioni 20 au zaidi, anakatwa kodi kwa utaratibu huu.

Kiwango hicho cha kodi cha asilimia 30% kwa mujibu wa sheria za kodi ya mapato, ndiyo kiwango cha juu zaidi kuliko kiwango kingine chochote. Kwenye kodi kuna viwango vya asilimia tano, asilimia 10%, asilimia 15%, asilimia 20%, asilimia 25% na asilimia 30% ambacho ndiyo kiwango cha mwisho kwenye kodi ya mapato.

Mfumo wa kodi ya ajira, unamtaka mwajiriwa alipe kodi kadri anavyopata kipato (PAYE). Mwajiriwa anayepata kipato kidogo, pia analipa kodi kidogo na anayepata kipato kikubwa na kodi pia huwa kubwa.

Kuhusiana na punguzo la kodi Serikali kila mara imekuwa ikirejea viwango vya kodi na kuendelea kuvipunguza ili kuongeza watu wengi zaidi kwenye wigo wa kodi.

Viwango vya kodi vinapokuwa juu sana, vinawafanya watu kukwepa kodi na ndiyo maana Serikali huvirejea viwango hivyo kila mara. Kwa zamani asilimia ya kodi ya ajira ilikuwa kubwa, kwa kuwa ilianzia asilimia 17% baadaye ikashushwa hadi asilimia 15%, ikashushwa tena hadi asilimia 14%, baadaye asilimia 12% na 11%, na sasa ni asilimia 9%.

Matokeo ya punguzo la asilimia 9% la kodi ya ajira, alilolitoa Rais John Magufuli, linaonekana zaidi kwa watu wenye kipato cha chini, tofauti na wenye kipato kikubwa.


For more detail and English Version  CLICK HERE


Labels:

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home